Ijumaa 5 Juni 2026 - 23:00
Marekani imebakiwa na wiki moja tu kabla ya kuingia katika mdororo wa uchumi

Hawza/ Mark Zandi, mwanauchumi mkuu wa taasisi ya Moody's Analytics, ameonya kwamba; iwapo juhudi za kidiplomasia na Iran hazitafanikiwa katika siku zijazo, kuongezeka kwa bei ya mafuta na nishati kunaweza kuusukuma uchumi dhaifu wa Marekani kuelekea katika mdororo wa uchumi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, ikinukuu Islamic Analysis, mwanauchumi mkuu wa taasisi ya Moody's Analytics ameonya kwamba; ikiwa suluhisho la kidiplomasia na Iran halitapatikana katika siku za karibuni, ongezeko kubwa la gharama za mafuta linaweza kuuingiza uchumi dhaifu wa Marekani katika mdororo wa uchumi.

Wakati kuendelea kwa vita dhidi ya Iran kumesababisha kupanda kwa bei za nishati na kuuweka uchumi wa Marekani katika hatari zinazoongezeka, mmoja wa wachumi mashuhuri wa Marekani ameonya kwamba; kuendelea kwa mshtuko katika soko la mafuta kunaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kutokea kwa mdororo wa uchumi.

Mark Zandi, mwanauchumi mkuu wa taasisi ya Moody's Analytics, katika mahojiano yake na Bloomberg alisisitiza kwamba; Marekani ina muda mfupi wa kuzuia madhara mabaya yatokanayo na kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta ghafi na petroli.

Akieleza kwamba masoko ya kifedha yanatarajia kupatikana kwa maendeleo ya kidiplomasia katika suala la Iran kunaweza kupunguza shinikizo katika soko la kimataifa la nishati, alisema: “Hili linapaswa kutokea katika siku chache zijazo au kwa kiwango cha juu zaidi hadi wiki ijayo, vinginevyo, nadhani tutakabiliwa na tatizo kubwa sana.”

Mlango wa Hormuz na ukingo wa mgogoro wa mafuta

Wakati huo huo, huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu uwezekano wa kutokea kwa hitilafu katika njia za usafirishaji wa baharini katika Ghuba ya Uajemi na athari zake kwenye usambazaji wa mafuta duniani, wachambuzi wameelekeza macho yao kwenye Mlango wa Hormuz, moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani.

Zandi alionya kwamba; kuendelea kwa bei za juu za mafuta kutawawekea mzigo mkubwa watumiaji wa Marekani, kutapunguza kiwango cha matumizi ya familia na hatimaye kusababisha shughuli za kiuchumi kupungua kasi.

Alieleza kuwa bei ya zaidi ya dola 5 kwa kila galoni ya petroli ni “kiwango cha hatari,” na akaongeza: “Ikiwa bei ya petroli kwa kila galoni itafikia dola 5, jambo hilo pekee litatosha kuusukuma uchumi wa Marekani ambao tayari ni dhaifu kuingia katika mdororo wa uchumi.”

Mwanauchumi mkuu wa Moody's, akitegemea takwimu za Idara ya Taarifa za Nishati ya Marekani (EIA), alikumbusha kwamba; akiba ya kimkakati ya mafuta ya Marekani imepungua hadi mapipa milioni 365, kiwango ambacho ni cha chini zaidi katika miaka miwili iliyopita.

Pia alionya kwamba; kupanda kwa bei ya mafuta ghafi na kuvuka dola 125 kwa kila pipa kunaweza kuwa ishara nyingine kubwa ya hatari inayoweza kuongeza uwezekano wa mdororo wa uchumi.

Wasiwasi wa masoko kuhusu Tehran

Tahadhari hii imetolewa wakati ambapo kumekuwa na ripoti kuhusu uwezekano wa Tehran kusimamisha mazungumzo na kuingilia shughuli za usafirishaji wa baharini ikiwa matakwa ya Iran hayatatekelezwa.

Shirika la habari la Tasnim jumatatu liliripoti kwamba; Tehra, hasa iwapo mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon yataendelea, inakusudia kusitisha mazungumzo na kuufunga Mlango wa Hormuz hadi hali inayotakiwa na Iran itakapopatikana.

Msimamo huu uliongeza wasiwasi uliokuwepo katika masoko na mwanzoni mwa wiki ulisababisha kupanda ghafla kwa bei ya mafuta.

Kwa msingi huo, bei za viwango vyote viwili vya mafuta vya Brent na West Texas Intermediate (WTI) ziliongezeka kwa takribani asilimia 7 asubuhi ya Jumatatu.

Hata hivyo, saa chache baadaye na kufuatia madai ya Donald Trump, rais wa Marekani, kuhusu kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon na kuzuiwa kwa shambulio la Israel dhidi ya Beirut, masoko yalitulia kwa kiasi fulani.

Baada ya kauli hizo, bei ya mafuta ilipoteza sehemu ya ongezeko lake, lakini bado iliendelea kubaki katika kiwango cha juu, karibu na dola 95 kwa kila pipa.

Muda unaisha kwa kasi

Kampuni ya ushauri wa masuala ya nishati ya HFI Research pia imeonya kwamba; iwapo mkwamo wa kidiplomasia hautatatuliwa, muda wa kuzuia madhara ya kiuchumi yatokanayo na mgogoro wa nishati unaisha kwa kasi.

Katika uchambuzi uliotolewa na kampuni hiyo imeelezwa: “Hatari iko karibu sana; chaguo zinaendelea kuisha na muda wa Trump unakaribia kuisha, ikiwa hadi mwisho wa mwezi Juni Mlango wa Hormuz utaendelea kufungwa, basi kupungua kwa usambazaji wa mafuta duniani hadi kiwango cha chini kabisa cha kiutendaji kutakuwa jambo lisiloepukika.”

Mashaka kuhusu kutokea kwa mdororo bado yanaendelea

Pamoja na tahadhari hii, bado hakuna makubaliano kamili kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mdororo wa uchumi nchini Marekani.

Katika muktadha huo, uchambuzi uliotolewa na tawi la New York la Benki Kuu ya Marekani (Federal Reserve) mwishoni mwa mwezi Aprili ulionyesha kwamba; viashiria vya soko la hati fungani vinatabiri uwezekano wa asilimia 17 pekee wa kutokea kwa mdororo wa uchumi wa Marekani katika miezi 12 ijayo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha